Polisi kuwasaka waliohusika kuwaua wanandoa Moshi

0
5

Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro linawasaka watu waliohusika katika mauaji ya watu wawili ambao ni wanandoa, Geofrey Mota (60), aliyeuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali shingoni pamoja na mke wake, Blandina Ngowi (53) ambaye mwili wake haukukutwa na majeraha.

Mauaji hayo yametokea nyumbani kwao Mtaa Msufini, Kata ya Msaranga, Wilaya ya Moshi Manispaa Mei 29, 2025 majira ya saa 1 jioni.

“Tukio hilo limetokea ndani ya nyumba ya kupanga waliyokuwa wakiishi wanandoa hao pamoja na kijana wao wa kiume (jina limehifadhiwa) ambaye ametoweka baada ya mauaji hayo kutokea,” imesema taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi.

Jeshi la Polisi limesema linaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha tukio hilo pamoja na kuwakamata wote waliohusika.

Aidha, miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya rufaa KCMC Moshi kwa uchunguzi na taratibu zingine.