Polisi kuwasaka waliotoa taarifa ya mgomo Kariakoo

0
51

Jeshi la Polisi nchini limesema Uongozi wa Umoja wa Wafanyabiashara wa soko la Kariakoo umeeleza kuwa tangazo linalosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kufunga biashara kuanzia Juni 24, 2024 hadi changamoto za wafanyabiashara zitakapotatuliwa halijatoka kwao na hata uongozi wao ngazi ya Taifa hawajathibitisha tangazo hilo kutoka kwao.

Akitoa taarifa hiyo leo jijini Arusha Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini Naibu kamishna wa Polisi DCP David Misime amesema Jeshi la Polisi linawahakikishia wafanyabiashara na wananchi wote kwa ujumla ambao wanafanya shughuli zao za biashara na kupata mahitaji katika soko hilo kuwa ulinzi utaimarishwa ipasavyo katika maeneo yote huku likabainisha kuwa wakati walio kula njama, kuandaa na kusambaza tangazo hilo wakitafutwa.

DCP Misime amesema kuwa mbali na tangazo hilo kutokujulikana limetolewa na nani, amebainisha kuwa limeenda mbali zaidi hadi kukiuka sheria za nchi kwa kutangaza vitisho kwa wafanyabiashara watakaokaidi agizo hilo kuwa mshale wa jicho utakuwa haki yake.

Jeshi la Polisi limewaomba wananchi kuendelea na shughuli zao kama kawaida bila hofu na kutoa wito kwa mtu yeyote mwenye changamoto zenye kuhitaji utatuzi afuate utaratibu wa kuzifikisha kwenye mamkaka husika ili zifanyiwe kazi na sio kuvunja sheria kwa kutoa vitisho na kulazimisha wengine kutekeleza yale ambayo hawakubaliani na waliotoa tangazo hilo.

Send this to a friend