Polisi: Mauaji mengi mwaka 2020 yamesababishwa na wivu wa mapenzi
Jeshi la Polisi limesema kuwa kwa kiasi kikubwa mauaji ya watu yaliyotokea nchini kwa mwaka 2020 yamesababishwa na wivu wa mapenzi na wananchi kujichukulia sheria mkononi.
Hayo yameelezwa katika taarifa ya jeshi hilo iliyotolewa na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Liberatus Sabas, ikiangazia hali ya ulinzi na usalama wa nchi.
Sabas ameeleza kuwa kutokana na hali hiyo, polisi wamekuwa wakitoa elimu kwa wananchi kutojichukulia sheria mikononi, na kuwataka viongozi wa dini kutoa elimu kwa waumini wao ili kusaidia kupunguza mauaji yatokanayo na wivu wa mapenzi.
Matukio mengine yaliyoangaziwa kwenye taarifa hiyo ni unyang’anyi wa kutumia silaha ambapo amesema matukio hayo yamepungua ikilinganishwa na mwaka ulioshia Novemba 2019. Katika mwaka huo kulikuwa na matukio 378 wakati kwa mwaka huu umekuwa na matukio 273, kukiwa na tofauti ya matukio 105.
Kuanzia Januari hadi Novemba 2019 kulikuwa na matukio ya ajali za barabarani 2,722 yaliyosababisha vifo vya watu 1,329. Kwa upande wa Januari hadi Novemba 2020 kumetokea ajali 1,800 zilizosababisha vifo vya watu 1,158.
Matukio mengine ni kuungua kwa shule ambapo jumla ya shule 31 zimeungua moto kati ya Januari na Novemba 2020, ambapo kati ya hizo, shule 20 ni binafsi na shule 11 ni za serikali.
Miongoni mwa sababu zilizochangiwa kuungua kwa shule hizo ni pamoja na hitilafu za umeme, migogoro shuleni na uzembe, polisi wameeleza.
Aidha, jeshi hilo limesema kumekuwepo na matukio ya wanafunzi kuacha shule na kujiunga na makundi ya kihalifu, miongoni mwa wahalifu hao ni wale waliokimbilia Msumbiji baada ya kupigwa na vyombo vya ulinzi mkoani Pwani.
Sabas amebainisha kuwa wamefanikiwa kuwakamata baadhi ya wanafunzi hao na wengine tayari wamevuka kwenda Msumbiji.
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi limewatala wananchi kuchukua tahadhari katika kupindi hiki cha sikukuu za mwisho wa mwaka, na kwamba watahakikisha raia na mali zao wanaendelea kuwa salama.