Polisi: Taarifa kuhusu viongozi wa upinzani kufanyiwa uhalifu ni za kutengeneza

0
28

Jeshi la Polisi nchini limesema taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zikieleza viongozi wa upinzani kufanyiwa vitendo visivyofaa hazina ukweli wowote bali ni taarifa za kutengeneza na kuongeza chumvi ili kupata huruma ya wananchi.

Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi imeeleza kuwa baada ya ufuatiliaji sambamba na kuchukua maelezo ya watu mbalimbali, imebaini taarifa ya mgombea wa Mtaa wa Miembeni Kilimahewa kupitia CHADEMA, Nsajigwa Mwandembwa kukamatwa na Polisi akiwa nyumbani, imebainika kuwa alikuwa akifanya fujo kwenye kituo cha kupigia kura na alionywa mara kadhaa lakini hakusikia na ndipo alikamatwa akiwa kituoni hapo, kisha kudhaminiwa ili kuendelea na taratibu za uchunguzi.

“Kuhusiana na taarifa aliyotoa kuwa Herman Lutambi Mzee amepigwa na Diwani wa CCM hadi kuvunjwa mkono, ufuatiliaji wa kina umefanyika na imebainika kilichokuwepo ni mzozo baina yao kulikosababisha kuchaniana shati na wala hakuvunjwa mkono kama Mwenyekiti huyo anavyodanganya,” imeeleza taarifa.

Imeongeza kuwa “kuhusu taarifa kuwa kulikuwa na jaribio la kumteka Christopher Kapaso, taarifa hizo zimefuatiliwa na hazina ukweli wowote.”

Aidha, Jeshi la Polisi limetoa wito kwa baadhi ya viongozi kama wana taarifa za kweli juu ya kufanyiwa uhalifu wowote wa kijinai waziwasilishe kuptia taratibu zilizopo za kisheria na kujiepusha kutengeneza taarifa zisizo za kweli kwa nia ya kuihadaa jamii.

 

 

 

 

Send this to a friend