Polisi: Taarifa ya kukamatwa Makamu Mwenyekiti ACT inaongezewa chumvi

Jeshi la Polisi mkoani Lindi limesema taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii ya kukamatwa kwa Mgombea Ubunge Jimbo la Lindi Mjini kupitia ACT-Wazalendo ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa chama, Isihaka Mchinjita, zingine zinaongezewa chumvi na kupotoshwa tofauti na ukweli uliopelekea kukamatwa kwake.
Kiongozi huyo wa chama alikamatwa Septemba 06, 2025 majira ya saa moja usiku wakati anatoka kwenye mkutano wa kampeni kwenye Viwanja vya Mpilipili, Lindi Mjini.
Jeshi la Polisi limefafanua kuwa ACT-Wazalendo kilikuwa na ratiba ya kufanya mkutano wa kampeni kwenye viwanja hivyo, na kabla ya kufanyika kwa mkutano, chama hicho kiliwasilisha taarifa kwa Mkuu wa Polisi wilayani Lindi kwamba wanataka maandamano kuanzia ofisini kwao kupitia stendi kuu ya mabasi, Soko la Zamani, Benki ya CRDB na kisha kuelekea viwanja vya mkutano kupitia Barabara ya Msinjahili, umbali wa zaidi ya kilomita nne.
“Baada ya kupokelewa kwa taarifa hiyo, Katibu wa ACT-Wazalendo Jimbo la Lindi Mjini aliitwa ofisini kwa Mkuu wa Polisi wilayani Lindi na kujulishwa kwamba taarifa ya kufanya maandamano imekataliwa,” imesema.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa baada ya kukataliwa ombi lao, viongozi na wafuasi wa chama walihamasishana na kutekeleza azma yao kwa kuandamana baada ya mkutano kumalizika, na ndipo Jeshi la Polisi lilipolazimika kutumia nguvu kuwatanya na kumkamata Makamu Mwenyekiti wa chama hicho na wenzake sita ambao waliachiliwa kwa dhamana baada ya mahojiano.






