
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewatoa hofu wananchi juu ya taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu mabaki ya viungo vya binadamu kudaiwa kukutwa eneo la Mpiji Magoe, Dar es Salaam, ambapo limesema tukio hilo ni la zamani, miaka 11 iliyopita.
Taarifa ya Jeshi la Polisi imetoa ufafanuzi kuwa watu wanne wakiwemo madaktari na wataalamu wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU) kilichopo Kunduchi, walikamatwa baada ya uchunguzi.
“Kukamatwa kwao kulitokana na taarifa za wananchi zilizopatikana kuwa katika bonde mto Mbezi eneo la Mpiji Magoe. Kulikuwa na viungo mbalimbali vya miili ya binadamu na baada ya Polisi kufika eneo lile na uchunguzi kufanywa kwa kushirikiana na mamlaka mbalimbali, ilibainika viungo vile vilikuwa vimetolewa kwenye maabara ya mafunzo ya chuo cha IMTU na kwenda kutupwa eneo lile kinyume na sheria.
Baadaye wahusika wakiwemo madaktari na wataalamu wa chuo hicho walifikishwa mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kinondoni na kusomewa mashitaka,” imesema taarifa.
Aidha, Jeshi la Polisi limewatahadharisha watu wenye tabia ya kutoa taarifa zenye malengo ya kuzua taharuki na kujenga hofu kwa umma kuwa halitasita kuchukua hatua za kisheria.







