
Gari la mgombea udiwani wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Igwachanya, Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe, Anthony Mahwata, limechomwa moto usiku wa kuamkia leo.
Tukio hilo limetokea saa 10 alfajiri ya leo wakati gari hilo lenye namba za usajili T633 ASH aina ya MITSUBISHI, likiwa gereji kwa ajili ya matengenezo.
Kamanda wa Polisi mkoani humo, ACP Mahmoud Banga amesema tukio hilo linaendelea kuchunguzwa ili waliohusika Kutenda tukio hilo wakamatwe na kufikishwa mahakamani.
“Bado kuna hisia kwamba nimefanyiwa hiki na fulani, sisi tunaendelea kuchunguza. Jeshi la Polisi tunakamata pale ambapo tuna uhakika kwamba mtuhumiwa huyu katenda, lakini kwa mfumo ulivyo hivi sasa wa haki jinai, tunachunguza kwanza ili tunapomkamata mtu basi baada ya hapo anafikishwa mahakamani moja kwa moja,” amesema Kamanda.








