
Jeshi la Polisi mkoani Geita limesema linachunguza na kufuatilia kwa ukaribu tukio la mwimbaji wa nyimbo za injili, Elisha Juma, mkazi wa Mtaa wa Kadisi, Kata ya Katente, Tarafa ya Ushirombo, Wilaya ya Bukombe kudaiwa kuchukuliwa na watu wasiojulikana.
Taarifa za kuchukuliwa kwa mwimbaji huyo zimeripotiwa katika Kituo cha Polisi Bukombe ambapo inadaiwa kuwa majira ya saa 10:00 jioni akiwa studio inayofahamika kwa jina la MAS J iliyopo Mtaa wa Kilimahewa, Kata ya Bulangwa alichukuliwa na watu watatu waliokuwa na gari nyeupe ambayo pia haikufahamika usajili wake na kuondoka naye kusikojulikana.
“Wakati tukio hilo linatokea, watu wengine waliokuwepo studio na mazingira hayo hawakuweza kutoa taarifa sehemu yoyote mpaka zilipowasilishwa Kituo cha Polisi na baada ya kuwasilishwa, hatua za uchunguzi kuhusiana na tukio hilo zimeanza mara moja,” imeeleza taarifa.
Jeshi la Polisi limetoa rai kwa yeyote mwenye taarifa za kuweza kusaidia kupatikana kwa Elisha asisite kuziwasilisha ili zifanyiwe kazi.
Aidha, limetoa rai kwa wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi kutoa taarifa sahihi na kwa wakati kuhusiana na tukio lolote la uhalifu ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa mara moja.







