
Jeshi la Polisi Tanzania limethibitisha kuanza uchunguzi wa kina kufuatia kusambaa kwa picha mjongeo inayomwonesha raia wa kigeni mwenye asili ya China akiwa na mifuko ya sandarusi iliyojaa fedha taslimu, zikiwemo fedha za ndani na za kigeni.
Tukio hilo linadaiwa kutokea nyumbani kwake katika eneo la Oysterbay, Mtaa wa Mazengo, nyumba za Phoenix, jijini Dar es Salaam baada ya majirani na viongozi wa serikali ya Mtaa kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, amesema uchunguzi tayari umeanza na kwamba taarifa kamili itatolewa baada ya hatua za uchunguzi kukamilika ili kubaini ukweli wa tukio hilo.
Picha mjongeo hiyo iliyosambaa mitandaoni inamuonesha raia huyo wa kigeni akiwa amezungukwa na watu wanaodhaniwa kuwa maafisa wa usalama waliovaa kiraia, wakimpa maelekezo ya kuzitoa fedha hizo kutoka kwenye mifuko mitatu ya sandarusi.








