
Jeshi la Polisi limesema limeanza kufanya uchunguzi tukio la mtia nia wa udiwani kata ya Sirari kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Sinda Samson Mseti (48) mfanyabiashara na mkazi wa kijiji cha Buriba Wilaya ya Tarime mkoani Mara ambaye anadaiwa kukamatwa na watu wasiojulikana.
Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Polisi Tarime Rorya imesema kwa mujibu wa mashuhuda, tukio hilo lilitokea Mtaa wa Nkende wilayani humo, na kwamba watu waliofanya ukamataji huo walikuwa na gari ndogo nyeupe aina ya Rasco yenye namba za usajili ya Kenya ambazo hawakuweza kuzitambua.
“Baada ya kupokea taarifa hiyo, Jeshi la Polisi limeanza uchunguzi wa kina kwa kupata maelezo ya mashuhuda wa tukio hilo, na uchunguzi unaendelea kwa lengo la kubaini wahusika ili hatua stahiki za kisheria zichukuliwe dhidi yao,” imesema taarifa.
Aidha, Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi kama kuna mwenye taarifa ya kuweza kusaidia kukamilisha upelelezi mapema asisite kuziwasilisha taarifa hizo ili zifanyiwe kazi.







