Polisi: Tunafuatilia kifo cha mwanafunzi wa UDOM aliyekufa maji kwenye maporomoko

0
21

Jeshi la Polisi mkoani Morogoro limesema linachunguza taarifa ya kifo cha mwanafunzi mmoja wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ambaye amekufa maji kwenye maporomoko ya maji Sanje yaliyopo katika Hifadhi ya Taifa ya Udzungwa, Kata ya Sanje, Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro.

Taarifa ya Polisi imesema tukio hilo limetokea Desemba 22, 2024, majira ya mchana ambapo Hezekiel Petro (21) ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa UDOM anayesoma masomo ya Sanaa na Historia, alikufa maji baada ya kukanyaga jiwe lenye utelezi na kutumbukia kwenye maji yenye kina kirefu.

“Mwanafunzi huyo alifika katika maeneo hayo akiwa kwenye ziara ya mafunzo kwa vitendo na wanafunzi wenzake zaidi ya 300 wakiwa wamefuatana na wakufunzi wao. Mwili wa mwanafunzi huyo ulitolewa kwenye maji na wataalam wa kuogelea na taratibu zingine za uchunguzi zinaendelea,” imesema taarifa ya Polisi.

Aidha, Jesh la Polisi limetoa wito kwa wananchi wote kuchukua tahadhari na kufuata maelekezo ya wataalam wanapotembelea maeneo yenye upekee.