Polisi: Tunafuatilia mazingira ya kupotea kwa kiongozi wa CHADEMA

0
60

Jeshi la Polisi limesema linafuatilia taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ya kupotea kwa kiongozi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jimbo la Vwawa, Hussein Mwashambwa kutokana na utata uliogubika mazingira yake.

Aidha, Jeshi la Polisi limesema kinachoendelea kuzungumzwa kwenye mitandao kwamba Mwashambwa alitekwa kwa kuwa alihamia CHADEMA, ni taarifa zinazohitaji kuthibitishwa na uchunguzi unaoendelea.

“Taarifa kamili itatolewa baada ya kupata maelezo kutoka kwake, watu wengine wenye ukweli wa mazingira ya tukio hilo ikisaidiwa na uchunguzi wa kisayansi,” imeeleza taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi.

Katika akaunti ya Twitter (zamani X), mmoja wa wanachama wa CHADEMA, anayetumia akaunti ya Mdude CHADEMA aliandika kuwa kiongozi huyo anayedaiwa kuwa alipotea kwa muda wa siku moja, alipatikana katika pori la Senjele, Mbozi akiwa katika hali ya kupoteza fahamu na kukimbizwa hospitalini.