Polisi: Tunawashikilia wafuasi wa CHADEMA kwa kufanya mikusanyiko isiyo halali

Jeshi la Polisi mkoani Mbeya limewakamata wafuasi sita wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Wilaya ya Rungwe mkoani humo akiwemo Mwenyekiti wa jimbo hilo, Gideon Mwakila kwa tuhuma za kufanya mikusanyiko isiyo halali ili kufanya maandamano ya kuadhimisha Siku ya Mashujaa kimkoa.
Taarifa iliyotolewa na Jeshi hilo imesema watuhumiwa hao walikamatwa Septemba 07, 2025, majira ya saa 6:30 mchana katika Kijiji cha Ndaga wilayani humo, huku wakiwa wamevalia sare za chama hicho pamoja na mabango.
Imeongeza kuwa watuhumiwa hao walitumia mbinu ya kupita mmoja mmoja kama wanaenda kwenye ibada, lengo likiwa ni kufanya maandamano hayo ambayo hayakufuata taratibu za kisheria.
“Uchunguzi unaendelea kukamilishwa ili hatua nyingine za kisheria ziweze kufuatwa,” imesema.
Aidha, Jeshi la Polisi limetoa wito kwa viongozi mbalimbali vya siasa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo.







