Polisi: Tundu Lissu hakuwa na ratiba ya kampeni Tarime

0
40

Jeshi la Polisi limetoa ufafanuzi kuhusu madai kuwa mkutano wa kampeni wa mgombea Urais wa CHADEMA, Tundu Lissu huko Nyamongo mkoani Mara ulisambaratishwa na jeshi la polisi Septemba 28 mwaka huu.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Tarime/Rorya amesema kuwa kwa mujibu wa ratiba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) tarehe tajwa mgombea huyo wa urais wa Tanzania alikuwa na safari ya kwenda Arusha kupitia Serengeti, lakini hakuwa na ratiba ya kuendelea na kampeni.

“Kimsingi siku ya tarehe 28 hakuwa na ratiba yoyote ya kufanya mkutano wa kisiasa ndani ya jimbo la Tarime Mjini na Tarime Vijijini,” amesema kamanda huyo.

Polisi wameeleza kuwa mgombea alibadili ratiba na kusimama njiani kuzungumza na wananchi na ghafla watu walianza kurushia mawe magari ya polisi, ndipo wakalazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya ili kunusuru usalama wao na msafara wa Lissu. Kufuatia tukio hilo watu wanne wanashikiliwa na polisi kwa mahojiano.

Jeshi hilo limewataka wanasiasa kufuata ratiba ya NEC ili kuepusha mgongano na vyama vingine ambapo zao lake ni uvunjifu wa amani pamoja na wananchi kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani na kwamba polisi wanaendelea kutoa ulinzi wakati wote.

Send this to a friend