Mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda, Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine amesema kuwa polisi nchini humo wamechukua fomu zake za kuwania kuteuliwa kugombea Urais, kufuatia upekuzi waliofanya kwenye ofisi yake Jumatano jioni.
Miongoni mwa nyaraka alizoripoti kuibwa ni fomu zenye saini za wadhamini milioni sita ambazo alitakiwa kuziwasilisha tume ya uchaguzi ikiwa ni sehemu ya vigezo vya mgombea kuweza kuteuliwa.
“Serikali ya Museveni inajaribu kunizuia nisiteuliwa kuwa mgombea Urais. Walianza kuhoji nyaraka zangu za elimu, umri wangu, sasa wanafanya kila jitihada kuvuruga uteuzi wangu na ninaamini hiyo ndiyo sababu ya wao kuchukua sahihi za wadhamini wangu.”
Mbali na nyaraka, amesema polisi wamechuka shilingi za Uganda milioni 23 (TZS milioni 14.4), fedha ambazo zilitarajiwa kuwasaidia wagombea ubunge wa chama chake katika mchakato wa uteuzi.
Mwanasiasa huyo ambaye amenuia kumuondoa Rais Yoweri Museveni madarakani baada ya miaka 34 ya kuiongoza Uganda amesema hatokata tamaa na tayari amewasiliana na mawakala wake zoezi la kukusanya sahihi za wadhamini lianze upya, ambapo mwisho wa kuwasilisha fomu hizo ni kesho Oktoba 16, 2020.
Hata hivyo tume ya uchaguzi imesema suala la kuchukuliwa kwa nyaraka za mtia nia huyo hazijafika mezani kwao, na kwamba mtia nia anaweza kuongezewa muda endapo atawasilisha hoja za msingi kwa tume hiyo.
Kupitia ukurasa wake wa Twitter, mwanasiasa huyo machachari amechapisha picha za askari polisi wakiwa katika ofisi yake na kusema kwamba tayari wamemaliza kufanya tathmini ya hasara iliyotakana na upekuzkli huo wa polisi.
Polisi wamekanusha kuzungumzia kiundani tukio hilo, lakini wamesisitiza kuwa msako huo haukuwa wa kisiasa.