Polisi waanza uchunguzi tukio la kushambuliwa kwa Ole Sendeka

0
17

Jeshi la Polisi limeanza uchunguzi juu ya tukio la kushambuliwa kwa risasi gari la Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka akiwemo ndani pamoja na dereva wake.

Tukio hilo lilitokea Machi 29, 2024 katika kijiji cha Ngabolo wilayani Kiteto, Mkoa wa Manyara wakati Ole Sendeka akiwa safarini kutoka Dodoma kwenda jimboni kwake Simanjiro mkoani humo, lakini yuko salama.

“Polisi wanafuatilia tukio hilo kwa ukaribu sana na uchunguzi umeshaanza baada ya kupokea taarifa, timu ya watalaamu wa uchunguzi inayohusisha matumizi ya risasi kutoka makao makuu ya polisi Dodoma imetumwa kushirikiana na timu ya mkoa wa Manyara kuchunguza kwa kina tukio hilo ili kubaini waliohusika kina nani au kusudio lao ni nini,” imeeleza taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Polisi Tanzania, David Misime.

Misime amesema baada ya uchunguzi wa kina unaofanywa na Jeshi la Polisi, taarifa rasmi zitatolewa.

Akizungumza na Mwananchi hapo jana, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Lucas Mwakatundu alisema hakuna mhusika yeyote wa tukio hilo aliyeshikiliwa na kwamba uchunguzi unaendelea.

Send this to a friend