Polisi waanza uchunguzi waombolezaji kuchoma magari yaliyosafirisha mwili wa marehemu

0
59

Jeshi la Polisi mkoani Morogoro limesema linafanya uchunguzi wa tukio la kuchoma na kuharibu magari mawili katika Wilaya ya Mvomero yaliyokuwa yakisafirisha mwili wa marehemu.

Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi imesema tukio hilo limetokea Desemba 17, 2025 katika Kata ya Diongonya, Tarafa ya Turiani wilayani Mvomero, ambapo gari yenye namba T. 214 EJU aina ya Mazda CX-5 na T. 350 DCH aina ya Toyota Noah yalichomwa moto na kuharibika na waombolezaji wa msiba.

“Magari hayo yalitumika kusafirisha mwili wa marehemu Mwanahasan Hamis (18) mfanyakazi wa kazi za ndani mkazi wa Turiani, aliyefariki kwa maradhi jijini Dar es Salaam kisha kusafirishwa kwenda mkoani Morogoro kwa shughuli za mazishi.

Wakati taratibu za mazishi zikiandaliwa, ilitokea taharuki iliyohusishwa na kutiliwa mashaka ya mazingira ya kifo cha marehemu, hali iliyosababisha kuchomwa kwa magari hayo na kuwafungia ndani wasindikizaji wa msiba ili watoe maelezo zaidi, imesema taarifa.

Taarifa imeeleza kuwa Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na uongozi wa Serikali za Mitaa waliweza kuwaokoa wasindikizaji wa msiba waliofungiwa huku ikianzisha uchunguzi wa kina kuhusu mazingira ya kifo hicho.

Send this to a friend