Polisi wakanusha kuhusika na kifo cha Babu G

0
53

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limekanusha taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zikidai polisi kuhusika kumuua Robert Mushi maarufu Babu G aliyepatika akiwa amehifadhiwa katika hospitali ya Polisi iliyopo Temeke.

Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi imesema Aprili 11, mwaka huu saa 10 alfajiri, askari polisi wa usalama barabarani alipokea taarifa kuwa eneo la taa za kuongozea magari Buguruni, Ilala, mwanaume mmoja aliyekuwa akivuka barabara kuelekea Chama aligongwa na gari ambalo halikusimama na kumsababishia majeraha sehemu mbalimbali za mwili.

“Mtu huyo alipelekwa Hospitali ya Amana na polisi, lakini baada ya kumfikisha madaktari walibaini kuwa alikuwa amefariki. Kwa sababu chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Amana hakikuwa na nafasi, ilishauriwa akahifadhiwe kwenye hospitali ya Jeshi la Polisi iliyopo barabara ya Kilwa, Temeke ambayo inatoa huduma hata kwa raia kuhusiana na suala hilo.”

Imeongeza kuwa “tarehe 21, 2024, ndugu wa marehemu walipatikana na wakautambua mwili wa ndugu yao kwani hakuwa na kitambulisho wala simu. Taratibu za mwisho za mazishi zinafanywa ili azikwe.”

Aidha, Jeshi la Polisi limesema litawachukulia hatua za kisheria mtu anayejiita Malisa gj na Bonoface Jacob ambao wamekuwa wakisambaza taarifa hizo kwenye mitandao yao kuwa mtu huyo ameuawa na polisi na kuzua taharuki kwa wananchi.

Send this to a friend