
Jeshi la Polisi mkoani Pwani limekanusha taarifa inayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu gari la Jeshi la Polisi kumgonga mwananchi eneo la Korogwe, Kibaha na kusababisha kifo chake, likiwataka wananchi kupuuza taarifa zinazosambazwa pasipo kuwa na uthibitisho wa mamlaka husika.
Polisi wameeleza kuwa Desemba 19, 2025 majira ya saa 2:00 usiku eneo la Kongowe barabara kuu ya Morogoro- Dar es Salaam gari ambalo halikutambulika namba za usajili lilimgonga mwanamke aliyefahamika kwa jina la Pendo Mashauri (20), mkulima na mkazi wa Kongowe na kumsababishia majeraha.
“Hata hivyo ajali hiyo haikuripotiwa kwa wakati katika kituo chochote cha Polisi badala yake ilipelekwa taarifa hiyo na shemeji yake aitwaye Kelvin Leonard tarehe Desemba 22, 2025 majira ya saa 12: 00 jioni,” imeeleza taarifa.
Polisi wamesema baada ya ajali hiyo, wananchi walimkimbiza majeruhi katika kituo cha afya cha White Hope kilichopo Miembesaba, Kibaha ambapo alipatiwa huduma ya kwanza kisha kuhamishiwa hospitali ya Rufaa ya Tumbi kwa matibabu zaidi ambapo Desemba 20, 2025 majira ya saa 9:00 usiku alifariki akiwa anaendelea kupatiwa matibabu.
Aidha, Jeshi la Polisi limesema hakuna shuhuda aliyethibitisha kutambua aina ya gari ambalo lilimgonga mwanachi huyo, hivyo linaendelea na msako mkali ili kuweza kubaini gari lililosababisha ajali hiyo.







