
Polisi mjini Kisumu nchini Kenya wanamsaka mwanamke anayedaiwa kumchoma kisu na kumuua mwanamke mwingine aliyeshukiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mume wake katika eneo la Nyamasaria, Kisumu Mashariki.
Mtuhumiwa, anayejulikana kama Rosemary Achieng maarufu kama Mama Boy, alimkuta marehemu, Brenda Awuor (30) akizungumza na mume wake katika kituo chake cha bodaboda.
Kwa mujibu wa ripoti ya polisi, mtuhumiwa alikuwa na kisu na alimdunga Brenda mara kadhaa kifuani kabla ya kutoroka. Brenda alifariki kutokana na kupoteza damu nyingi.
Aidha, uchunguzi unaonyesha kuwa marehemu alikuwa mfanyabiashara wa M-Pesa karibu na kituo cha bodaboda ambako mume wa mtuhumiwa, John Ayima, alikuwa akifanya kazi.
Mashahidi wanasema kuwa John alikuwa na uhusiano wa kimapenzi wa wazi na marehemu, jambo ambalo huenda lilimkasirisha mke wake.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Jaramogi Oginga Odinga, huku polisi wakiendelea kumsaka mtuhumiwa aliyekimbia baada ya tukio.