Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango ametoa siku saba kwa vyombo kuhakikisha wahalifu waliotekeleza mauaji ya watu wa tano wa familia moja katika Kijiji cha Zanka, wilaya ya Bahi mkoani Dodoma wanapatikana.
Akiwasilisha rambirambi kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan, Dkt. Mpango ameoneshwa kusikitishwa na kitendo cha mauaji ya wanafamilia hao licha ya kuwepo kwa majirani wengi wanaozunguka eneo hilo.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais ameliagiza jeshi la Polisi nchini kuchukua hatua kukomesha vitendo vya mauaji yanayojitokeza hapa nchini, na kwamba hivi karibuni maeneo mbalimbali ya nchi vimeibuka vitendo vya mauaji hivyo ni lazima wahusika kuchukuliwa hatua kali za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine.
Amemuagiza Mkuu Wilaya ya Bahi pamoja kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo kufanya mkutano na wananchi wa eneo hilo ili kuimarisha ulinzi wa maeneo hayo.
Aidha ameuagiza uongozi wa Kijiji cha Zanka kufanya vikao vya mara kwa mara juu ya ulinzi na usalama wa maeneo hayo.
Akizungumza katika mkutano na wana kijiji wa eneo hilo amewasihi wananchi wa Kijiji cha Zanka na Watanzania kwa ujumla kutafuta namna ya kutatua migogoro ikiwemo kutumia vyombo vya sheria badala ya kufanya matukio ya mauaji.
Pia amewaomba viongozi wa dini kuendelea kutoa mafundisho ya kukemea vitendo vya uhalifu ikiwemo mauaji hapa nchini.