Jeshi la Polisi linawashikilia Polisi watano wa kituo kidogo cha Uyole jijini Mbeya kwa tuhuma za kula njama na kutaka kusafirisha wahamiaji haramu sita raia wa Ethiopia.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 3, 2022, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amesema tukio hilo lilitokea Oktoba 20, 2022 na Jeshi lilipata taarifa za siri kutoka kwa raia wema ambao walitaja namba za gari lililotumika kuwasafirisha wahamiaji hao kutoka Mbeya mjini kwenda Wilaya ya Kyela mpakani wa Tanzania na Malawi.
“Baada ya kufuatilia tulibaini gari aina ya Toyota mali ya askari ambaye ni miongoni mwa askari wanaoshikiliwa,” amesema.
Kamanda Kuzaga amewataja askari wengine na namba zao kuwa ni ASP Thomas Mbwile, G 3132 Koplo Beda, G 3146, Koplo Mohammed, G6364 Koplo Joseph wote wa Kituo cha Polisi Uyole.
Aidha, mesema watuhumiwa hao wanaendelea kushikiliwa kwa mahojiano zaidi na watafikishwa mahakamani wakati wowote mara baada ya uchunguzi kukamilika.
“Natoa ovyo kwa watumishi wa Serikali ambao wanajihusisha na tabia ya kusafirisha wahamiaji haramu watambue kuwa Jeshi ka Polisi halijalala na watawajibishwa kwa mujibu wa Sheria”ameeleza.