Jeshi la Polisi lafanikiwa kumpata binti aliyefanyiwa ukatili, wanne washikiliwa
Jeshi la Polisi limesema limefanikiwa kumpata binti aliyeonekana kwenye video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii akifanyiwa ukatili, na kwa sasa amehifadhiwa eneo salama na anaendelea kupatiwa huduma zinazostahili mtu aliyefanyiwa ukatili wa aina hiyo.
Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi imesema imebaini kuwa tukio hilo lilifanyika eneo la Swaswa katika jiji la Dodoma mwezi Mei 2024 na sasa limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wanne kati ya sita ambao walipanga na kutekeleza uhalifu huo .
“Watuhumiwa hao wamekamatwa mkoani Dodoma na Mkoa wa Pwani ambao ni Clinton Damas maarufu ‘Nyundo’, Praygod Mushi, Amini Lema na Nickson Jackson,” imeeleza taarifa.
Aidha, limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wanne kutoka Dar es Salaam waliosambaza picha mjongeo (video clip) wa tukio hilo kwenye mitandao ya kijamii ambao ni Frora Mlombora, Aghatha Mchome, Medatha Jeremiah na James Paulo.
Mbali na hao, watuhumiwa wengine wanne wamekamatwa kwa tuhuma za kutengeneza na kusambaza taarifa za uongo mtandaoni zikieleza kuwa binti huyo amefariki pamoja na mama yake, ambapo watuhumiwa wawili wamekamatwa huko Arusha na wawili mkoani Dar es Salaam.
Jeshi la Polisi limeeleza kuwa uchunguzi unaendelea pamoja na kuendelea kuwasaka watuhumiwa wawili ambao bado wamejificha ili wafikishwe mahakamani.