Polisi yakanusha Bobi Wine kupigwa risasi, yadai alijikwaa

0
21

Polisi nchini Uganda wamekanusha madai kwamba kiongozi wa upinzani, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, alipigwa risasi Jumanne jioni, badala yake, wamesema kwamba kiongozi huyo wa National Unity Platform (NUP) alijeruhiwa wakati akijaribu kuingia kwenye gari lake.

Kwa mujibu wa msemaji wa polisi, Kituuma Rusoke, amesema maafisa wa polisi waliokuwepo eneo hilo wanadai kuwa Bobi Wine alijikwaa wakati akijaribu kuingia kwenye gari lake na kupelekea jeraha hilo, ingawa Bobi Wine na timu yake wanasisitiza kuwa alipigwa risasi.

Polisi wamesema Bobi Wine alikuwa akirejea kutoka kwenye sherehe ya kumshukuru wakili wa NUP, George Musisi huko Bulindo, Kira Municipality, Wilaya ya Wakiso, wakati alipokumbana na tukio hilo.

Taarifa ya Polisi inaeleza kuwa Bobi Wine na timu yake walipanga maandamano hadi mji wa Bulindo licha ya polisi kupiga marufuku maandamano hayo. Katika mvutano huo, imedai kuwa alijeruhiwa, huku wakieleza kufanya uchunguzi ili kubaini ukweli wa tukio hilo.

Taarifa hii inafanana na tukio la Januari 2021 huko Fort Portal, ambapo Luteni Jenerali Henry Tumukunde alidaiwa kupigwa risasi kwenye mguu wa kushoto, lakini jeshi lilikanusha. Tumukunde alidai kuwa alitofautisha kati ya risasi na bomu la machozi, lakini msemaji wa jeshi alidai kuwa jeraha lilisababishwa na bomu la machozi.

Send this to a friend