
Jeshi la Polisi mkoani Singida limekanusha kumkamata na kumshikilia Shekhe Zuberi Nkokoo (53), mwalimu wa dini ya Kiislam kutoka Taasisi ya Islamic Foundation ambaye ameripotiwa kupotea Juni 02, 2025 saa 5:30 usiku akiwa karibu na Sheli ya Lake Oil iliyopo Mtaa wa Misuna, Singida.
Aidha, Jeshi hilo limesema linawashikilia watu watatu kwa mahojiano ambao ni Abdul Ally (58), mkazi wa Arusha, Shabani Ikenga (54) mkazi wa Singida na Maulid Mussa (52) mkazi wa Arusha ambao wote ni wafanyabiashara.
“Jeshi la Polisi linaendelea kufanya uchunguzi kubaini mahali alipo mtu huyo ili kujua kama amekamatwa au ameshikiliwa, mhusika ni nani na sababu za kushikiliwa kwake,” imesema taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi
Jeshi la Polisi limewataka wananchi kupuuza taarifa za uzushi na za uongo zinazoenezwa kwa nia ya kuleta taharuki kwa jamii na badala yake watoe ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kubaini alipo kiongozi huyo.