
Jeshi la Polisi limemwelekeza aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole afike katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) ili aweze kutoa maelezo na ushahidi kuhusiana na tuhuma ambazo amekuwa akizitoa kupitia mitandao ya kijamii.
Taarifa iliyotolewa na Jeshi hilo imesema mbali na kukusanya ushahidi, limekuwa likifanya jitihada za kumpata ili aweze kutoa maelezo na vielelezo vitakavyothibitisha tuhuma hizo ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.
“Jeshi la Polisi Tanzania lingependa kutoa taarifa kuwa lilifungua jalada la uchunguzi na linaendelea kuchunguza tuhuma mbalimbali ambazo amekuwa akitoa Humphrey Polepole toka Julai 2025,” imeeleza.
Taarifa imeongeza kuwa “Tuhuma ambazo ametoa na anaendelea kuzitoa kulingana na jinsi alivyozielezea zinaashiria uwepo wa makosa ya jinai, na kwa mujibu wa sheria zinahitaji ushahidi wa kuthibitisha zitakapo wasilishwa mahakamani. “







