Polisi yapiga marufuku maandamano ya Desemba 9

0
51

Jeshi la Polisi limepiga marufuku maandamano yaliyopangwa kufanyika Desema 9, 2025, likisema kuwa yamekosa sifa za kisheria za kuyaruhusu kufanyika, ikiwemo kulenga uvunjifu wa amani.

Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi imeeleza kuwa ufuatiliaji wa kina umebaini mipango hatarishi inayoratibiwa mitandaoni na kupitia makundi ya watu wanaohamasisha maandamano hayo.

Imeongeza kuwa uchunguzi umeonesha kuwa wahamasishaji wa maandamano wanapanga mbinu mbalimbali hatarishi, ikiwemo kuwataka watu waliopata mafunzo ya silaha kuzitumia siku hiyo; kusimamisha shughuli zote, kuchoma minara ya mawasiliano ili kukatisha huduma, kufunga barabara zinazoelekea na kutoka Bandarini Dar es Salaam, pamoja na kufunga mipaka ya nchi.

Aidha, Jeshi la Polisi limeeleza kuwa hakuna barua yoyote iliyofikishwa au kupokelewa ya kutoa taarifa ya kufanyika maandamano hayo.

“Maandamano hayo yanayopewa jina la maandamano ya amani na yasiyo na kikomo yamekosa sifa za kisheria za kuruhusiwa kufanyika na kwakuwa yametangazwa kufanyika nchi nzima, kwakuwa hakuna barua yoyote iliyofikishwa au kupokelewa na ofisi yoyote na Mkuu wa Polisi wa Wilaya,” imeeleza taarifa.

Send this to a friend