
Mwanaume mmoja ambaye hajafahamika jina wala makazi yake anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 30 hadi 35, amekutwa kwenye mchanga wa ufukwe wa bahari akiwa hajitambui maeneo ya Coco Beach Oysterbay, Kinondoni, Dar es Salaam saa tano asubuhi, huku akiwa amefungwa bandeji ngumu ya muda mrefu (PoP) mkono wake wa kulia.
Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, imesema tukio hilo lilitokea Aprili 24, 2025 kisha taarifa kufikishwa Polisi na watu wanne wafanyabiashara ndogondogo wa eneo hilo, ambao pia hawamtambui mtu huyo ambaye alifikishwa Hospitali ya Mwananyamala ambako ilithibitika kuwa alikuwa amekwishafariki dunia.
“Maiti hiyo imehifadhiwa Hospitali ya barabara ya Kilwa kutokana na matatizo ya nafasi ya kuhifadhi hospitali ya awali,” imesema taarifa.
Aidha, Jeshi la Polisi limesema linaendelea na uchunguzi juu ya chanzo cha kifo hicho.