
Jeshi la Polisi mkoani Kigoma limesema watu watatu waliokuwa majambazi wameuawa baada ya majibizano ya risasi na Askari Polisi wakati wakifanya jaribio la unyang’anyi wa kutumia silaha.
Taarifa ya Polisi imesema tukio hilo limetokea Julai 31, 2025 saa 3:00 usiku eneo la Kumshindwi katika kijiji cha Kigendeka, Wilaya ya Kibondo mkoani humo, ambapo askari polisi wakiwa kwenye doria walidhibiti tukio hilo, ambapo majambazi walifunga barabara ya Kibondo-Kasulu kwa mawe kwa lengo la kufanya unyang’anyi.
“Katika majibizano hayo ya risasi, majambazi watatu ambao bado hawajatambuliwa kwa majina wala anwani za makazi wameuawa baada ya kujeruhiwa kwa risasi. Miili ya marehemu imehifadhiwa Hospitali ya Kibondo kwa utambuzi,” imeeleza taarifa.
Aidha, Jeshi la Polisi limesema limekamata silaha moja, AK 47, magazini moja ikiwa na risasi 10, silaha za jadi, bunduki moja iliyotengenezwa kienyeji, visu viwili, panga moja na marungu matatu.








