Polisi yawashikilia watu 18 kwa tuhuma za kufanya mikusanyiko kinyume na sheria

0
104

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linawashikilia watu 18 akiwemo Katibu Mwenezi wa Baraza la Vijana Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Felius Festo Kinimi kwa tuhuma za kufanya mikusanyiko kinyume na sheria na kuhamasisha vurugu.

Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro imesema tukio hilo limetokea maeneo ya Sambarai Kibosho Wilaya ya Moshi Septemba 06, mwaka huu.

“Jeshi la Polisi limekuwa likiwafuatilia sambamba na kukusanya ushahidi na leo walipokuwa wanakwenda kutekeleza vitendo ambavyo ni kinyume cha sheria ndiyo likafanikiwa kuwatia nguvuni,” imeeleza taarifa.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa ushahidi unaendelea kukamilishwa ikiwa ni sambamba na kuwahoji watuhumiwa ili hatua zingine za kisheria ziweze kuchukuliwa.

Jeshi la Polisi limetoa onyo kwa yeyote anayepanga njama za kuhamasisha na kufanya vurugu ili kuhatarisha amani, utulivu na usalama hasa katika kipindi cha uchaguzi na baada ya uchaguzi kuwa halitasita kuwakamata ili sheria ziwezi kuchukua mkondo wake.

Send this to a friend