Polisi Zanzibar wasema hakuna sheria ya kukamata wanaokula mchana Ramadhani

0
56

Jeshi la polisi Zanzibar limesema hakuna sheria inayowaruhusu Polisi Zanzibar kuwakamata watu wanaokula hadharani mchana katika kipindi cha mwezi Ramadhani.

Kamishna Mkuu wa Jeshi la polisi Zanzibar, CP Hamad Khamis Hamad amefafanua kuwa lengo la polisi lilikuwa ni kuwakamata watu waliokuwa wakivuta bangi maeneo ya Mnazi Mmoja baada ya kupokea kipande cha video kikiwaonesha watu hao pamoja na wengine waliokuwa wakila mchana.

Serikali ya Zanzibar yalaani unyanyasaji unaofanyika kwa sababu za kidini

“Kuna vijana walikuwa Mnazi Mmoja wanavuta bangi mchana, na kwa bahati nzuri ni kwamba aliyekuwa anarekodi alikuwa anazungumza kwamba watu wanavuta bangi mchana wanakula mchana kwa hiyo kilichofanyika nilitoa maelekezo kwamba ifanyike operesheni wale wavuta bangi kwa sababu ni kosa la jinai. Shida iliyojitokeza operesheni hii nadhani ilikamata waliomo na wasiokuwemo yaani wavuta bangi na wengine ambao walikuwa wanakula mchana,” ameeleza.

Ameongeza “tunafahamu kwamba kunakuwa na operesheni wakati mwingine zinafanyika kwa mamlaka nyingine za Kiserikali huwa zinafanya oparesheni hizo, wajibu wetu sisi kama Jeshi la Polisi ni kusimamia operesheni za aina hiyo ili zifanyike kwa usalama na amani.”

Send this to a friend