PPRA: Serikali imepata hasara ya TZS bilioni 8

0
13

Ripoti ya ukaguzi na uchunguzi iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) imebainisha kuwa Serikali imepata hasara ya jumla ya TZS bilioni 8.77 kutokana na ukosefu wa uwajibikaji, ufanisi, uwazi na uadilifu kwenye taasisi 12 zilizochunguzwa.

Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande akizungumza mara baada ya kupokea ripoti ya Tathmini ya Utendaji ya PPRA kwa mwaka wa Fedha 2022/23 iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi PPRA, Dkt. Leonada Mwagike ameziagiza mamlaka husika ikiwemo TAKUKURU kuzichukulia hatua stahiki taasisi zote zilizokiuka sheria, kanuni, na miongozo iliyowekwa.

Katika ripoti hiyo, Dkt. Mwagike amesema mamlaka ilifanya ukaguzi kwa taasisi nunuzi 180 ukihusisha wizara, idara za serikali zinazojitegemea, wakala za Serikali, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa pamoja na mashirika ya umma.

Nchi 10 za Afrika zenye kiwango cha juu zaidi cha mfumuko wa bei

“Kati ya taasisi nunuzi 180 zilizokaguliwa, taasisi 28 zilikuwa na matokeo ya kuridhisha, taasisi 109 zilikuwa na matokeo ya wastani na taasisi 43 zilikuwa na matokeo hafifu. Kati ya taasisi hizo 43, taasisi 28 zilikuwa kwenye kundi la Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, taasisi 8 zilikuwa kundi la mashirika ya umma na tasisi 7 kwenye kundi la wizara, idara za serikali zinazojitegemea na wakala za Serikali,” amesema.

Aidha, ripoti hiyo imeeleza kuwa serikali imeokoa fedha za umma zenye thamani ya shilingi bilioni 2.26 zilizotokana na kurejeshwa kwa malipo ya awali, kodi ya ongezeko la thamani na kuzuia kwa malipo yaliyokiuka utekelezaji wa mikataba.

Send this to a friend