Precision Air yasitisha safari zake kwenda Kenya

0
47

Kampuni ya Ndege ya Precision Air yenye makazi yake nchini Tanzania imetangaza kusitisha kwa muda safari za kwenda Nairobi nchini Kenya kwa kile ilichoeleza kuwa ni kutokuwepo kwa abiria wa kutosha.

Katika taarifa iliyochpishwa kwenye ukurasa wa Twitter, kampuni hiyo imewaomba radhi wateja wake huku ikieleza kuwa itatangaza tarehe ya kuanza kwa safari hizo na kuwataka wale wenye tiketi kufika kwenye ofisi za mauzo kufanya mabadiliko.

Uamuzi wa Precision Air umekuja siku chache baada ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Kenya kueleza kuwa hawatazuia ndege hiyo ya Tanzania kuingia nchini humo kama ambavyo Tanzania imezuia makampuni matatu ya ndege ya Kenya kuingia nchini.

Tanzania na Kenya zimekuwa katika mvutano wa safari za anga ambapo hivi karibuni mashirika matatu ya ndege ya Kenya, AirKenya Express, Fly540 na Safarilink Aviation yalizuiwa kufanya safari zake nchini kutokana na mvutano unaoendelea baina ya nchi hizo.

Hatua ya Tanzania ilifuatia serikali ya Kenya kutangaza orodha ya nchi 130 ambazo raia au wageni kutoka nchi hizo hawatowekwa karantini siku 14 waingiapo Kenya, lakini Tanzania haikuwa miongoni mwa nchi hizo.

Send this to a friend