Precision Air yatuma wataalam kufanya uchunguzi wa ajali ya ndege

0
57

Uongozi wa Precision Air kupitia Mkurugenzi Mkuu, Patrick Mwanri umesema umetuma watu wao kwenda Bukoba ili kufanya uchunguzi kujua nini chanzo cha ajali ya ndege katika Ziwa Victoria mkaoni Kagera.

Akizungumza na vyombo vya habari amesema ndege hiyo iliondoka Dar es Salaam saa 12 alfajiri na walitarajia kuwasili Bukoba saa 2:30 asubuhi lakini ilipofika saa 2:53 walipokea taarifa kwamba ndege haijawasili na kwamba imepata ajali ziwani.

“Kwa taarifa nilizonazo mpaka sasa watu 26 wameokolewa na wamekimbizwa Hospitali, jitihada za kuokoa abiria waliosalia zinaendelea pale Bukoba, vikosi vyetu vyote viko pale Katika kuhakikisha watu wote wanaokolewa, tunaendelea na mawasiliano kuhakikisha suala hili kinafanyika kwa haraka.” amesema.

Aidha, amesema wamefungua kituo maalum kwa ajili ya kusaidia familia za wahanga katika hoteli ya ELCT Bukoba ili kuwapa taarifa mbalimbali, na kwa Dar es Salaam kituo kitakuwa hoteli ya Blue Sapphire Vingunguti.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka eneo la tukio, miili ya watu watatu imetolewa ndani ya ndege, huku zoezi la uokoaji likiendelea.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa anatarajiwa kwenda wilayani Bukoba kuungana na wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama katika zoezi la uokoaji.

Send this to a friend