
Prince Harry amesema anatamani kurudisha uhusiano mzuri na familia yake ya kifalme, hasa baba yake Mfalme Charles, ambaye anaugua saratani na hazungumzi naye, kwa sababu hajui ni kwa muda gani baba yake ataendelea kuishi.
Harry, ambaye anaishi Marekani na familia yake, ameshindwa kesi ya kupinga uamuzi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uingereza ya kuondoa ulinzi wake baada ya kujiondoa kwenye majukumu ya kifalme.
Prince Harry amesema haiwezekani kumrudisha mkewe Meghan na watoto wao Uingereza kwa sasa kwa sababu hana ulinzi wa kutosha, baada ya kushindwa katika kesi ya kupinga kuondolewa kwa ulinzi binafsi aliyokuwa akipewa akiwa nchini humo, akiongeza kuwa bado anaipenda Uingereza na ana huzuni kwamba hatoweza kuwaonyesha watoto wake nchi alikokulia.
Kuhusu mgogoro wake wa kifamilia, Prince Harry amesema “Kumekuwa na kutokuelewana na tofauti nyingi kati yangu na baadhi ya wanafamilia wangu. Hali hii ya sasa, ambayo imeendelea kwa miaka mitano, inahusu masuala ya uhai na usalama, ndiyo kikwazo pekee kilichosalia.
“Ni wazi kuwa baadhi ya wanafamilia wangu hawatanisamehe kamwe kwa kuandika kitabu, wala mambo mengine mengi niliyoyafanya, lakini… ningependa sana tupatane tena kama familia.”
Aidha, ameeleza kuwa hatalalamika tena kisheria, akisema kwamba uamuzi uliotolewa siku ya Ijumaa umeonesha kuwa hakukuwa na njia yoyote ya kushinda kupitia mahakama.