Prof. Kabudi: Awamu ya pili ya Rais Magufuli atajikita kuboresha sekta binafsi

0
14

Serikali imesema katika kipindi cha muhula wa pili wa miaka mitano ya Rais Dkt. Magufuli itajikita zaidi katika diplomasia ya uchumi, kuimarisha sekta binafsi, kukuza biashara pamoja na mahusiano na mataifa mengine duniani.

Msimamo wa Tanzania umetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi wakati wa mkutano wake na Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa Tanzania pamoja na wakuu wa mashirika ya kimataifa na kuongeza kuwa ni dhamira ya Tanzania kuhakikisha kuwa ina uwezo wa kukuza biashara na kuuza bidhaa katika nchi mbalimbali duniani.

“Katika mwaka huu unaoanza sasa na miaka ijayo katika mhula wa pili awamu ya tano ni wakati muafaka wa Tanzania kuimarisha diplomasia ya uchumi na uhusiano mwema baina yake na nchi mbalimbali kwa kuwakaribisha wawekezaji kutoka nchi hizo katika maeneno ya uzalishaji, viwanda na kuongeza biashara kwa manufaa ya mataifa yote,” amesema Prof. Kabudi

Prof. Kabudi ameongeza kuwa hali ya kisiasa na amani Zanzibar na Tanzania kwa ujumla imeimarika kuliko wakati wowote hususani mara baada ya uchaguzi mkuu uliomalizika Oktoba, 2020 na kwamba uwepo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar unachochea kuongezeka kwa uwekezaji na ufanyaji wa biashara kwa lengo la kukuza uchumi.

Kwa upande wake Kiongozi wa Mabalozi, Dkt. Ahmada El Badasui ambaye pia ni Balozi wa Comoro hapa nchini ameshukuru kwa uwepo wa mkutano huo ambao unawapa fursa mabalozi kufahamu masuala mbalimbali yanayoendelea hapa nchini.

Kwa upande wake Balozi wa Umoja wa Ulaya, Manfredo Fanti ameipongeza Tanzania kwa kuingia uchumi wa kati na kwamba Umoja wa Ulaya uko tayari kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha Uchumi wa Tanzania unaendelea kukua na kuimarika.

Send this to a friend