Prof. Mkumbo: Serikali itaendelea kufanya ufuatiliaji mali za serikali zilizopo chini ya Ofisi ya Hazina

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo amesema serikali itaendelea kufanya tathmini na ufuatiliaji wa mali za serikali zilizopo chini ya usimamizi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina pamoja na zile zilizobinafsishwa, ikiwemo mashamba, viwanda, nyumba na viwanja.
Ameyasema hayo wakati wa mapendekezo ya Bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka ujao wa fedha ambapo amewasilisha mbele ya Bunge vipaumbele vitano vya Ofisi ya Hazina vinavyolenga kuongeza ufanisi wa taasisi za umma, usimamizi wa rasilimali za umma na kukuza mapato yasiyo ya kodi hadi TZS trilioni 1.56.
Prof. Mkumbo amesema OMH itaanza kutekeleza mpango wa muda mrefu wa miaka 25 wa usimamizi wa mali za serikali hadi 2049/50. Mpango huo unalenga kutoa dira ya kiuchumi na uwekezaji wa kitaifa.
Ameongeza kuwa, Ofisi ya Msajili wa Hazina iko kwenye mchakato wa kufanya maboresho makubwa kwenye matumizi ya TEHAMA kwa kuandaa Dash bodi ambayo itarahisisha utekelezaji wa majukumu. Maboresho hayo yatawezesha upatikanaji wa takwimu kwa wakati, kuongeza uwazi na kurahisisha usimamizi wa mapato yasiyo ya kodi.