Puma Energy Tanzania Yaunga Mkono Maadhimisho ya Siku ya Samia kwa Kuchangia Nishati Safi ya Kupikia

0
5

Kampuni ya Puma Energy Tanzania leo imeungana na wakazi wa mkoa wa Dodoma katika kusherehekea Siku ya Samia, ikiwa ni kuenzi uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, hususan katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa Watanzania.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary S. Senyamule (kati) akipokea mitungi ya gesi ya kupikia kutoka kwa Jeffrey Nasser, Mkuu wa Kitengo cha Mauzo Nishati Safi kutoka Puma Energy Tanzania, kama sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kuendeleza matumizi ya nishati safi ya kupikia. Kushoto ni James Kigodi, Meneja wa Kanda ya Kati Puma Energy Tanzania. Tukio hili lilifanyika tarehe 3 Juni jijini Dodoma.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Bi. Fatma Abdalla, Mkuu wa Kitengo cha Mauzo ya Nishati Safi wa Puma Energy Tanzania, Bw. Jeffrey Nasser, alikabidhi rasmi mitungi ya gesi kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mheshimiwa Rosemary S. Senyamule, kama sehemu ya kushiriki katika tukio hilo muhimu.

“Ushiriki wetu leo ni uthibitisho wa dhamira ya Puma Energy kushirikiana na serikali katika kuhakikisha nishati safi inamfikia kila Mtanzania. Puma Gas, tangu ilipozinduliwa mwaka 2022, inalenga kubadilisha maisha kwa kuondoa matumizi ya nishati hatarishi,” alisema Bw. Nasser.

Tangu kuanzishwa kwa kampeni ya nishati safi mwaka 2024, matumizi ya gesi nchini yameongezeka kutoka asilimia 6 hadi asilimia 16 ndani ya mwaka mmoja — mafanikio yaliyotokana na juhudi za pamoja kati ya serikali na wadau kama Puma Energy.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Senyamule, alitoa shukrani kwa kampuni ya Puma Energy kwa mchango wake mkubwa: “Siku ya Samia ni siku ya kutafakari mafanikio makubwa yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais wetu. Tunawashukuru Puma Energy kwa kuwa sehemu ya mafanikio hayo kupitia mchango wao wa gesi safi ya kupikia.”

Amesisitiza kuwa ajenda kuu ya siku hii ni kuhamasisha matumizi ya nishati safi, na kwamba Puma Energy imeonyesha mshikamano mkubwa katika kutekeleza maono haya ya kitaifa.