Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA), Gianni Infantino amezishutumu nchi za Magharibi kwa unafiki kutokana na namna zinavyoripoti kuhusu masuala ya haki za binadamu na msimamo wa Qatar juu ya watu wanaojihususha na mapenzi ya jinsia moja.
Infantino amesema hayo saa chache kabla ya kuanza kwa mashindano ya Kombe la Dunia nchini humo, mashindano ambayo yamegubikwa na masuala mengi yanayoihusu Qatar ikiwa ni pamoja na vifo vya wafanyakazi wahamiaji waliohusika katika maandalizi ya mashindano hayo.
Infantino ambaye ni mzaliwa wa Uswizi amesema kuwa mataifa ya Ulaya yanapaswa kuomba radhi kwa vitendo vilivyofanywa katika historia zao, badala ya kuzingatia masuala ya wafanyakazi wahamiaji nchini Qatar.
Amesema “Kwa kile ambacho sisi nchi za Ulaya tumekuwa tukifanya kwa miaka 3,000 iliyopita tunapaswa kuomba msamaha kwa miaka 3,000 ijayo kabla ya kuanza kutoa masomo ya maadili kwa watu.”
Mnamo Februari 2021, gazeti la Guardian lilisema wafanyakazi wahamiaji 6,500 kutoka India, Pakistan, Nepal, Bangladesh na Sri Lanka walifariki nchini Qatar tangu iliposhinda zabuni yake ya Kombe la Dunia,
Hata hivyo Qatar imepinga takwimu hizo ikisema waliofariki ni 37 na kati yao, watatu tu ndio vifo vyao vinahusishwa na kazi waliyokuwa wakifanya, takwimu ambazo Shirika la Kimataifa la Kazi (ILO) ilizikanusha ikisema ni ndogo.