Raia 76 wa Ghana waliodanganywa kupewa ajira Nigeria waokolewa

0
121

Jeshi la Polisi la Ghana limethibitisha kuwa limewaokoa raia 76 wa Ghana waliokuwa wamesafirishwa kwenda nchini Nigeria kupitia mpango wa udanganyifu wa ajira unaohusishwa na kampuni ya masoko ya Q-NET.

Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (CID), Kamishna Msaidizi wa Polisi (DCOP) Lydia Yaako Donkor amesema waathirika waliahidiwa ajira nje ya nchi, mikataba ya kucheza mpira, na msaada wa kupata visa.

Taarifa zinaeleza kuwa washukiwa saba wa Ghana waliokuwa sehemu ya mtandao wa ulaghai huo pia wamekamatwa Nigeria na bado wanashikiliwa.

Waathirika wengi ni vijana wa kiume waliokuwa wakiishi katika mazingira duni, ambapo simu zao na hati za kusafiria zilichukuliwa walipowasili, na waliwekwa chini ya uangalizi mkali wakilazimishwa kuwasiliana na familia zao nchini Ghana kuomba pesa kwa madai ya ada za mafunzo au gharama za uratibu.

Amesema madhara ya kiuchumi na kisaikolojia kwa waathirika na familia zao ni makubwa sana, hivyo amewaomba raia wa Ghana kuwa waangalifu na matangazo ya ajira au mafunzo nje ya nchi yanayohitaji malipo ya awali au yanayofanywa bila nyaraka rasmi.

Hatua zinaendelea kuchukuliwa ili kuwarejesha waathirika nyumbani Ghana na kuwaunganisha na familia zao. Aidha, washukiwa wengine waliokamatwa Ghana kutokana na mtandao huo huo wa ulaghai tayari wamefikishwa mahakamani.

Send this to a friend