Paul Hendrik van Zyl (77) raia mzungu aishie Afrika Kusini amefikishwa Mahakamani baada ya kumpiga risasi na kumjeruhi mwanamke mweusi akidai kuwa alidhani mwanamke huyo ni kiboko.
Mwanaume huyo ambaye ni mmiliki wa shamba alikamatwa Aprili 26 baada ya kufyatua risasi akiielekeza kwa mwanamke huyo aliyekuwa akivua samaki na mpenzi wake kwenye mto katika mji wa Lephalale, Kaskazini mwa jimbo la Limpopo Afrika Kusini.
Aidha taarifa zinasema Ramakone Linah (38) muathirika wa tukio hilo alipata majeraha ya risasi kwenye mkono wake huku mpenzi wake akifanikiwa kujificha wakati wa tukio.
Hata hivyo kwa mujibu wa mamlaka ya kitaifa ya mashtaka (NPA) Hendrik anakabiliwa na mashtaka ya kujaribu kuua huku Mahakama ikimuachilia kwa dhamana ya randi 1,000 (sawa na shilingi za Kitanzania 145,649).
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 18 kwa ajili ya uchunguzi zaidi.