Raia wa China anaye wakaririsha na kuwarekodi watoto nyimbo za ubaguzi akamatwa

0
31

Msanii wa filamu kutoka nchini China, Lu Ke ambaye aliyekuwa akitafutwa na serikali ya Malawi kwa tuhuma za kuwakaririsha na kuwarekodi watoto nyimbo za ubaguzi wa rangi amekamatwa.

Mshukiwa huyo, alikuwa akisakwa kwa tuhuma za ubaguzi wa rangi na unyanyasaji wa watoto baada ya kuonyeshwa kwenye kituo cha runinga cha BBC.

Msemaji wa uhamiaji nchini Malawi Pasqually Zulu amesema mtuhumiwa amekamatwa katika nchi jirani ya Zambia na polisi wa Malawi siku ya Jumatatu alipokuwa akijaribu kutoroka kupitia njia ambazo hazijafahamika.

Zulu amesema kwa sasa Malawi inawasiliana na serikali ya China ili Lu Ke azuiliwe kwa muda mrefu ili kuruhusu mamlaka kukamilisha uchunguzi wao.

Inaelezwa kuwa katika video zake Lu Ke aliwalazimisha watoto waimbe nyimbo kwa lugha ya kichina ambayo ilikua na maneno ya kibaguzi bila wao wenyewe kuelewa.

Katika video moja, ambayo ilizua gumzo hadharani, kundi la watoto lilionekana likikariri wimbo wa Kichina ambao ulitafsiriwa kuwa “Mimi ni mnyama mweusi (black monster) na akili zangu ni ndogo.”

Kwa upande wake, mwanadiplomasia wa China Wu Peng alishikilia kuwa nchi yake haikubaliani na ubaguzi wowote dhidi ya mataifa mengine na itaendelea kuwakandamiza watu kama Lu Ke na kuhakikisha wanatiwa hatiani.

Send this to a friend