Katika hali ya kushangaza mamlaka nchini Nigeria zimesema kuwa hazifahamu ilipo timu ya madaktari 15 wa binadamu raia wa China iliyowasili nchini humo mapema Aprili mwaka huu.
Timu hiyo iliwasili nchini Nigeria kwa ajili ya kusaidia mapambano dhidi ya virusi vya corona, ambapo serikali ya China ilisema kuwa wataalam hao walikwenda kufuatia ombi la serikali ya Nigeria.
Mapema Mei 14, 2020 Waziri wa Afya wa Nigeria, Osagie Ehaire aliwaambia waandishi wa habari kuwa wataalam hao walikuwa wageni wa kampuni moja ya ujenzi, na sio wote walikuwa madaktari, huku akisema amesikia kwamba baadhi ni mafundi wa kampuni hiyo.
“Inaonekana kumekuwa na maswali mengi sana kuhusu madaktari hawa, lakini ni wafanyakazi wa kampuni. Nitakuwa na furaha sana kama mtaacha kuniuliza walipo,” alisema waziri huyo akionekana mwenye hasira.
“Hawakuwa wageni wetu kwa minajili hiyo, lakini tumeweza kujifunza mambo kadhaa kutoka kwao. Huwa tunashirikishana mawazo juu ya namna walivyoweza kukabiliana na covid-19 nchini mwao,” ameongeza Ehaire.
Hata hivyo kauli hiyo inaonekana kukinzana na iliyotolewa na Waziri wa Habari, Lai Mohammed wiki iliyopita ambapo alisema kuwa madaktari hao wanaendelea na shughuli katika vitu mbalimbali nchini humo kwa kuwajengea uwezo madaktari.
Wakati wageni hao wakiwasili makundi mbalimbali kikiwemo Chama cha Madaktari wa Nigeria (NMA) kilikosoa ujio huo, lakini serikali ilisisitiza kuwa watakuwa wakitoa usaidizi tu.