Raia wa India wajaribu kutoroka karantini kukwepa msongamano
Maelfu ya raia wa India waliowekwa karantini nchini humo wamelalamikia hali mbaya katika vituo hivyo ikiwemo kutokuwa na umbali wa kutosha kati ya mtu na mtu na chakula kisicho kizuri.
Awali katika vituo hivyo walikuwa wakiwekwa watu ambao vipimo vilionesha kwamba wana maambukizi ya virusi vya corona, lakini hawana dalili yoyote, watu waliokuwa karibu na watu wenye maambukizi pamoja na wale waliokuwa wamesafiri nje y nchi.
Lakini hali ilibadilika baada ya nchi hiyo kutangaza kuanza kwa ‘lockdown’ na kupelekea vituo hivyo kufurika watu waliokamatwa wakijaribu kutoroka miji ya Delhi, Mumbai, Ahmedabad iliyokuwa imefungwa.
Baadhi ya maafisa wanaosimamia vituo hivyo wameeleza kuwa hali si nzuri na kwamba watu wanahitaji vitanda bora, vyoo safi, na kwamba wao kama wasimamizi hawana cha kusaidia zaidi ya kuwataka kutulia.
Tangu Aprili 16 mwaka huu kumeripotiwa matukio 27 ya vurugu katika vituo mbalimbali vya karantini, vitendo ambavyo vinadaiwa kusababishwa na hofu na mazingira yasiyo rafiki kwa wananchi.
Aidha, watoa huduma za afya ambao wapo mstari wa mbele nao wameelezea mazingira magumu wanayofanyia kazi, ikiwemo zaidi ya watu 50 kutumia vyoo viwili.
Serikali imesema kuwa inafanya kila linalowezekana kuhakikisha watu hao wanakuwa salama, huku ikiwataka wananchi kuwa wavumilivu.
Hadi Aprili 26, India imeripoti visa zaidi ya 26,900 vya waathirika wa corona, ambapo kati ya waathirika hao, 5,939 wamepona huku waliofariki wakiwa ni 826.