Raia wa Nigeria jela miaka 28 kwa kusafirisha dawa za kulevya

0
36

Mahakama Kuu ya Uhujumu Uchumi, Divisheni ya Makosa ya Rushwa, imemhukumu David Kanayo Chukwu, raia wa Nigeria, kifungo cha miaka 28 jela baada ya kukiri kosa la kushiriki katika usafirishaji wa kilogramu 268.50 za dawa za kulevya aina ya heroin.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Otaru Joachimu amesema mahakama imezingatia kipindi cha miaka mitano na miezi tisa ambacho mshtakiwa huyo amekaa mahabusu tangu alipokamatwa. Kutokana na hilo, atatumikia miaka 22 na miezi mitatu iliyobaki ili kukamilisha adhabu yake.

Katika shauri hilo hilo, mahakama imemwondolea mashtaka mshtakiwa wa tatu, Alistair Amon Mbele, baada ya upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha hatia dhidi yake, huku mshtakiwa wa pili, Isso Lomward Lupembe, kesi yake inaendelea kusikilizwa baada ya kukana shtaka linalomkabili.

Aidha, mahakama imeelekeza shauri la kutaifishwa mali (asset forfeiture) zinazohusishwa na watuhumiwa hao lishughulikiwe ndani ya mwaka mmoja kuanzia tarehe ya kutolewa kwa hukumu.

Watuhumiwa hao walikamatwa na maafisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) mwaka 2020 eneo la Mbezi Kibanda cha Mkaa.

Send this to a friend