Raila Odinga asitisha maandamano ya Jumatano

0
21

Chama cha Azimio La Umoja One Kenya kimesimamisha maandamano yake dhidi ya serikali yaliyokuwa yamepangwa kufanyika nchi nzima siku ya Jumatano wiki hii.

Kupitia taarifa iliyotolewa leo, chama hicho kimesema badala ya kwenda mitaani, watashiriki maandamano ya mshikamano na maombi kwa ajili ya waathirika wa ukatili wa polisi katika maeneo mbalimbali nchini.

Chama kimewaomba wafuasi wake kujitokeza kwa wingi na kuwasha mishumaa na kutandaza maua kwa ajili ya watu waliopoteza maisha yao wakati wa maandamano.

Chama hicho kinachoongozwa na Raila Odinga, kimesema hadi sasa vifo 50 vimeripotiwa na wengine kadhaa wamejeruhiwa na wamelazwa hospitalini kutokana na majeraha mabaya.

“Tumeamua kwamba Jumatano badala ya kwenda mitaani kwa maandamano ya amani kama ilivyotangazwa awali, tutafanya maandamano ya mshikamano na maombi kwa ajili ya waathirika wa ukatili wa polisi katika maeneo mbalimbali nchini,” imesomeka taarifa hiyo.

“Tunawaomba Wakenya wajitokeze na kuwasha mishumaa na kutandaza maua kuwakumbuka na kuwaenzi waathirika. Wakati wa maandamano hayo, wakati tunawasha mishumaa na kutandaza maua, tunawahimiza Wakenya kuomba na kusoma majina ya waathirika wa ukatili wa polisi. Tutatoa orodha ya majina hayo kwa ajili ya zoezi hilo.”

Azimio pia imeomba viongozi wa kidini kutenga siku za Ijumaa, Jumamosi, na Jumapili kwa ajili ya maombi ya kuwakumbuka waathirika hao wakati wa maandamano ya amani yaliyofanyika hapo awali.

“Tunawaomba Wakenya pia kusali ili Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ichukue suala hili kwa kutumia orodha pana ya watu waliohusika ambayo tunakusudia kuwasilisha mahakamani baadaye,” imeongeza.

Send this to a friend