Rais aagiza Tume kuchunguza sababu na namna vurugu za Oktoba 29 zilivyodhibitiwa

0
82

Rais Samia Suluhu Hassan ameiagiza Tume Huru ya Uchunguzi wa Matukio ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025 kuchunguza sababau za vijana kuandamana na kufanya vurugu, pamoja na kujua ni haki gani waliyokuwa wakidai ili ifanyiwe kazi.

Ameyasema hayo leo wakati akizindua tume hiyo Ikulu, Jijini Dodoma ambapo amesema majibu ya tume hiyo ndiyo yataweka msingi wa ajenda na dira ya Tume ya Maridhiano aliyoiahidi kuiunda ndani ya siku 100 tangu kuingia madarakani.

“Tunaitarajia tume ikatuangalizie sababu hasa iliyoleta kadhia ile, sababu hasa ni nini? Kiini cha tatizo ni nini? Lakini jambo lile lilipotokea vijana waliingizwa barabarani kudai haki, tunataka kujua haki gani ambayo vijana wale wameikosa na kwa umoja wao waliingia barabarani kuidai haki hiyo,” amesema.

Aidha, Rais Samia ametoa wito kwa Tume kuchunguza pia taarifa zinazodai kuwa baadhi ya vijana walilipwa fedha kabla ya kushiriki maandamano, na kubaini chanzo cha fedha hizo pamoja na mchango wa mashirika ya ndani na nje ya nchi katika tukio hilo.

Pia, ameiagiza tume kuchunguza matamshi ya vyama vya upinzani yaliyoashiria uvunjifu wa amani, kuchunguza uhusiano baina ya vyama vya siasa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) pamoja na namna vurugu hizo zilivyodhibitiwa.

Amesema tukio la uvunjifu wa amani halikutarajiwa nchini kutokana na historia ya muda mrefu ya utulivu wa kisiasa na usalama ambayo Tanzania imeijenga tangu uhuru.

Send this to a friend