Rais Samia Suluhu amelielekeza Jeshi la Polisi kuhakikisha madereva wanaongeza umakini na kuzingatia sheria za barabarani hasa kipindi hiki cha mwisho wa mwaka ili kuepusha ajali zinazoweza kuepukika.
Akitoa salamu za pole baada ya ajali iliyoua watu saba na kujeruhi watu tisa wilayani Karagwe mkoani Kagera, amesema utekelezaji wa agizo hilo uende sambamba na uwekaji wa alama za barabarani kwenye maeneo hatarishi, pamoja na kuzingatia umbali na maeneo sahihi ya uwekaji wa vituo vya ukaguzi ili vionekane kwa urahisi zaidi.
Aidha, Rais Samia ameelekeza abiria na watumiaji wa barabara kutumia namba za simu za Makamanda wa Polisi wa Mikoa kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi, wakati wowote wanapoona viashiria vya uzembe na ukiukwaji wa sheria na alama za barabarani.