Rais atoa rai kwa Watanzania kuuenzi Mwenge wa Uhuru kwa kufanya kazi kwa bidii

0
49

Rais Samia Suluhu Hassan ametoa rai kwa vijana wa Kitanzania kuendelea kuulinda Mwenge wa Uhuru ambayo ni Tunu ya Taifa na kuuenzi kwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii.

Ameyasema hayo leo wakati wa Kumbukizi ya Miaka 25 ya Kifo cha Hayati Mwalimu Nyerere na Maadhimisho ya Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru yaliyofanyika katika Uwanja wa CCM Kirumba mkoani Mwanza, ambapo ametoa pongezi kwa vijana kwa ubunifu, ujuzi, uthubutu na utayari wao kupitia kazi zao huku akiwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kutatua changamoto zinazowakabili.

Aidha, Rais Samia ameeleza kuwa maono na fikra za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere zinaendelea kuishi, na taifa la Tanzania linaendelea kujivunia amani, mshikamano na umoja.

“Mzee wetu Mwalimu Nyerere alitujengea umoja wa kitaifa wa Watanzania, taifa lenye jamii za makabila zaidi ya 120, tunajivunia mshikamano na umoja wetu,” ameeleza Rais Samia.

Mbali na hayo, amewapongeza vijana walioshiriki mbio za Mwenge wa Uhuru za mwaka 2024 kwa kuzunguka nchi nzima kuhamasisha shughuli za maendeleo na kuwahimiza wananchi kufanya kazi kwa bidii, kuwajibika na kuwa wazalendo kwa taifa lao.

Vilevile, amewaeleza wananchi wa mkoa wa Mwanza kuwa kipande cha tano cha Reli ya Kisasa ya Umeme (SGR) kutoka Isaka – Mwanza, ujenzi wake unaendelea na umefikia asilimia 60 na Serikali inaendelea na utekelezaji ili kukamilisha asilimia 40 iliyobakia. “Hii ni kudhihirisha dhamira yetu ya kuhakikisha reli ya SGR inafika Mwanza, na dhamira hiyo itatimia si muda mrefu.”

Send this to a friend