Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia kutoa tani 189 za mbegu za mpunga, mahindi na alizeti ili zisambazwe kwa wakulima wa wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro.
Ameyasema hayo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akizungumza na wananchi wa maeneo ya Mlimba, Taweta, Masagati wilayani Kilombero, mkoani Morogoro ambako alikwenda kukagua athari za mafuriko.
“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatoa pole kwa wananchi wote walioathirika na mafuriko yaliyotokana na mvua zinazonyesha nchini, lakini pia ametoa mbegu hizo ili kuhakikisha wale waliopata athari katika mashamba yao waweze kuendelea na shughuli za kilimo pale hali itakapokaa sawa,” amesema.
Waziri Mkuu ambaye pia alikagua bonde la mto Kilombero linalojumuisha wilaya tatu za Kilombero, Ulanga na Malinyi, amesema Rais Samia ameelekeza Serikali iendelee kuwahudumia wananchi wote waliopata athari ikiwemo kuimarisha maeneo ya utoaji huduma za afya, kugawa vyakula na kurejesha miundombinu ikiwemo barabara na reli.
“Watanzania tuwe watulivu, Serikali yenu ipo kazini. Rais wetu Dkt. Samia ametupa maelekezo ya kuhakikisha tunawahudumia na kurejesha hali, tutaleta vyakula na tayari madaktari takribani 20 wameshasambazwa kwenye mikoa ya Morogoro na Pwani ili waweke kambi za utoaji huduma za afya,” ameeleza.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameziagiza TARURA, TANROADS na TAZARA zishirikiane kufanya ukarabati katika maeneo yote yaliyopata athari wakati Serikali inasubiri kumalizika kwa mvua ili iweze kufanya ukarabati mkubwa.